Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wakataa hali zao kukwamisha ndoto zao, sanaa yawainua

Noura Zainal(kulia), Msanii na bingwa wa Taekwondo akiwa na mwalimu wake Dkt. Zainab; Noora hakuruhusu Usonji kufunga ndoto zake.
UN News/Assumpta Massoi
Noura Zainal(kulia), Msanii na bingwa wa Taekwondo akiwa na mwalimu wake Dkt. Zainab; Noora hakuruhusu Usonji kufunga ndoto zake.

Vijana wakataa hali zao kukwamisha ndoto zao, sanaa yawainua

Na Assumpta Massoi - Bahrain
Malengo ya Maendeleo Endelevu

Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya wazazi kutelekeza mtoto aliyezaliwa na usonji au ugonjwa wa unaoathiri uwezo wa mtu kujifunza, Down Syndrome. Jambo ambalo Umoja wa Mataifa linapinga likitaka ujumuishwaji. Sasa  nchini Bahrain harakati za wazazi zimeshika kasi na zinazaa matunda.

Soundcloud

Imedhihirika wazi wakati wa jukwaa lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO, ofisi ya uendelezaji wa teknolojia, ITPO nchini Bahrain. Assumpta Massoi alikuwa ni shuhuda wetu.

Katika ushoroba  maalum kando ya ukumbi uliofanyika Jukwaa la Nne la Uwekezaji kwa Wajasiriamali, WEIF 2024 hapa Manama mji mkuu wa Bahrain, nashuhudia msanii akichora picha chini ya uongozi. Nikamsogelea akaniambia, naitwa Daniah Maroof, ninasomea ubunifu wa picha kwenye kompyuta katika Chuo Kikuu cha Wanawake Bahrain. Na pia napenda sanaa na hii nimefanya tangu nikiwa na umri mdogo. Familia yangu inapenda sana kuchora.

Daniah Maroof(kushoto), Msanii wa picha kwenye kompyuta katika Chuo Kikuu cha Wanawake Bahrain akiwa na mama yake.
UN News/Assumpta Massoi
Daniah Maroof(kushoto), Msanii wa picha kwenye kompyuta katika Chuo Kikuu cha Wanawake Bahrain akiwa na mama yake.

Dania ana usonji na mama yake huambatana naye kumsaidia na kumwongoza, na hapa akanieleza.

“Naitwa Hala Ahmed Sulaiman, mama wa mwanafunzi na msanii anayeibukia, Daniah Maroouf. Daniah ana umri wa miaka 24, imechukua miaka kadhaa kuboresha na kuendeleza kipaji chake. Tunashukuru msaada kutoka kwa mwalimu binafsi, pamoja na shule yake, Chuo Kikuu na matukio kama haya. Tusingalifika hatua hii ya leo.”

Shule ya Daniah ilikuwa na msaada gani? Mwenyewe akanieleza.

“Mwalimu wa sanaa aliuliza iwapo mtu anapenda kuchangia sanaa. Hivyo nikasema ndio na watu wengi walishiriki na kisha kuonesha sanaa zao. Watu wengi walinunua kazi zangu za sanaa na fedha tulipeleka kusaidia viziwi. Lakini baada ya onesho hili nilielekeza kuhamasisha kuhusu wagonjwa wa saratani. Nilipata takribani dinari 100,000 za Bahrain sawa  dola zaidi ya 265,000. Baada ya hapa nilishiriki mashindano ya Chuo Kikuu na imenisaidia sana na nimekuwa nashinda shuleni na hata Chuo Kikuu na sasa niko mwaka wa pili Chuo Kikuu.”

Nikaona picha ya msichana na nyingine ya ndege msituni, nikamuuliza anapata vipi wazo la kuchora?

“Ni ubunifu zaidi kuliko chochote kile. Kwa sababu unapochora unapaswa kuwa na taswira fulani kwenye fikra zako. Na pia napenda kucheza na rangi, inatokana na ubunifu wa kuchora kwenye kompyuta. Unapaswa kujua nini watu wanapenda.Picha hii inanikumbusha rafiki yangu wa shule kwa sababu ana nywele ndefu zenye mawimbi, na huu ndio muonekano wake, nilichora picha yake. Na ndege hawa wako kwenye mazingira asili. Ujumbe wangu watu waendelee kuchora picha shuleni. Kwa sababu zina ujumbe unaoweza kusoma.”

Pamoja na binti yake kuwa na usonji, Hala alihakikisha kipaji kinaendelea. Hivyo akatoa ujumbe kwa wazazi wengine.

Tweet URL

“Kwanza kabisa kama mama ana mtoto au watoto au yeyote kwenye familia mwenye mahitaji maalum lazima tuwaamini na kuwapatia msaada. Na iwapo mtu hana changamoto hiyo, basi tufundishe vizazi vijazo jinsi ya kuhudumia watu wenye mahitaji maalum, tuwaheshimu, tuwapatie fursa stahiki, na kuamini kwenye uwezo wao kwa sababu wao ni sehemu ya jamii bila kujali changamoto zao.”

Pembeni ya Daniah, kuna msanii mwingine amemakinika kabisa akichora picha ya mwanamke aliyevaa hijabu. Yeye mwenyewe kavaa hijabu. Nikiwa nasogea, akahisi kuna mtu nyuma yake, akageuka na kisha akatabasamu. Alinyanyuka na kunisalimia.. Kisha kunipatia kipeperushi cha kazi zake.

Kimeandikwa jina lake Noora Zainal, msanii wa kuchora na bingwa wa mchezo wa Taekwondo. Anapenda kuimba, kucheza dansi na kuwa na paka wake aitwaye Moza. Noora alizaliwa na ugonjwa unaothiri uwezo wa mtu kujifunza au Down Syndrome.

Alinyanyuka na kunipatia maelezoya michoro yake, moja farasi na nyingine ni mti wenye maua ya manjano. Nyingine ni jua likizama kwenye baharí.

Baada ya maagano akarejea kuendelea kuchora.

Dkt. Zainab Sarour, ni Mmiliki na Mkurugenzi wa Kituo cha Micro Art Studio ambako Noura ni mwanafunzi wa usanii. Dkt. Zainab ni mtaalamu wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum.

Lengo la kituo hiki ni kujumuisha watu wenye mahitaji maalum ambao pia wana vipaji kwenye dunia ya sanaa sambamba na wasanii wabobezi. Watu wenye mahitaji maalum wakishaonesha kupenda sanaa, tunawakuza na kuimarisha nafsi zao na kuwasaidia kutangamana na jamii. Pili tunalenga kuwasaidia wawe na malengo yao na miradi yao ambako watauza wao wenyewe sanaa zao bila kuhitaji msaada. Wanatengeneza kazi zao, wanashiriki maonesho, wanatafuta masoko na hatimaye wanapata kipato.”