Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli za chuki na mauaji ya kimbari ni lila na fila havitengamani: Nderitu

Alice Wairimu Nderitu mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari.
UN News/Assumpta Massoi
Alice Wairimu Nderitu mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari.

Kauli za chuki na mauaji ya kimbari ni lila na fila havitengamani: Nderitu

Amani na Usalama

Alice Wairimu Nderitu mashauri maalum wa Umoja wa Mataifa  katika kuzuia mauaji ya kimbari akizungumza na UN New Kiswahili hivi karibuni ametoa rai kuhusu mauaji hayo na uhusiano wake na kauli za chuki huku akimtaka kila mtu kumakinika na kuchukua hatua.

Bi. Nderitu anasema, “Ningependa watu wajue kwamba mauaji ya kimbari huwa hayafanyiki bila mpango. Na wenye kupanga huwa wanajua wale watu  wanaopanga kuwaangamiza ni lazima kwanza wawatoe utu , wawaonyeshe kwamba wao sio binadamu. Na ndio maana huwa wanaitwa mende kama walivyokuwa wakiwaita Watutsi, au chawa kama walivyowaita watu wa Rohingya au watu wachafu kama walivyokuwa wanawaita watu wa Yazid huko Iraq. Na kila mtu akisikia watu wanaitwa haya majina ya wanyaka inafaa wajue mpango unaweza kuwepo, na huo mpango unaweza kuwa ni wa mauaji ya kimbari.”

Akaenda mbali zaidi na kusisitiza,

“Kwa hivyo kila mtu achukulie kauli za chuki kwa uzito mkubwa. Kama tungependa kuishi kama watu walio na utu na tungependa kurejesha utu duniani , tuendelee kuwasaka walio na utu ndio tuweze kuwachukulia hatua wale wanaotoa kauli za chuki, kuzungumza nao na kuwafunza watoto na kufunza watu wengi kwenye hii dunia maana ya kauli za chuki sababu nisingependa watu wasahau ya kwamba hakuna mauaji ya kimbari  yalishafanyika bila kauli za chuki. Hatungependa yale yaliyofanyika Rwanda yatokee tena. Hivyo kama hatutaki yafanyike tena tukumbuke kwamba kauali za chuki zinatuelekeza sote kwenye mauaji ya kimbari.