Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumaini ya mwisho ya mustakbali bora Gaza ni ulinzi wa UNRWA: UN

Wajumbe kutoka Jordan, Kuwait na mataifa mengine yanayounga mkono wanatoa tamko la pamoja kuhusu Ahadi za Pamoja za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA). Miongoni mwa washiriki Kamishna Mkuu…
UN News
Wajumbe kutoka Jordan, Kuwait na mataifa mengine yanayounga mkono wanatoa tamko la pamoja kuhusu Ahadi za Pamoja za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA). Miongoni mwa washiriki Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini.

Matumaini ya mwisho ya mustakbali bora Gaza ni ulinzi wa UNRWA: UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerejea kusema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ndilo mhimili wa operesheni za kibinadamu huko Gaza na kwamba hakuna njia mbadala yake, akisisitiza kuwa kazi yake ni moja ya shughuli kubwa za kibinadamu ambazo hutoa mwanga wa matumaini na kipimo cha utulivu katika eneo hilo tete.

Akihutubia mkutano wa ahadi kwa ajili ya UNRWA, Guterres ameonya kwamba "bila ya msaada na ufadhili unaohitajika kwa UNRWA, wakimbizi wa Palestina watapoteza maisha muhimu na mwanga wa mwisho wa matumaini ya maisha bora ya baadaye."

Ameendelea kusema kuwa "Mwaka huu ni tofauti. Ni kweli kwamba tunakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili. Lakini Wapalestina pia wanakabiliwa na mapungufu makubwa kote. Wapalestina wa Gaza sio tu kwamba wanakabiliwa na mapungufu wamezingirwa na moto ambao unavuruga kabisa sheria na utulivu. Tulipofikiri kwamba hali ya Gaza haiwezi kuwa mbaya zaidi sasa raia wanasukumwa ndani zaidi kuliko hapo awali."

Amesisitiza kwamba hakuna kitu kilichohalalisha mashambulizi ya kutisha ya Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana, wala hakuna kitu chochote kinachohalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina.

Katibu Mkuu amesema sasa ni wakati wa kuhitimisha vita hivyo vya kutisha, kwa kuanzia na tangazo la usitishaji mapigano kwa minajili ya kibinadamu huko Gaza na kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa mateka wote.

Chakula chenye nguvu nyingi na virutubisho muhimu kinasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao huko Khan Younis, Gaza.
© WFP/Jaber Badwan
Chakula chenye nguvu nyingi na virutubisho muhimu kinasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao huko Khan Younis, Gaza.

Kuilinda UNRWA

Katibu Mkuu amesema kuwa wafanyakazi wenzake wa UNRWA hawajaepushwa na zahma ya vita hivyo ambapo wafanyakazi 195 wa UNRWA wameuawa ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi waliouawa katika muda mfupi katika historia ya Umoja wa Mataifa.

Amebainisha kuwa shirika hilo pia linalengwa kwa njia nyingine. "Je, unaweza kufikiria jinsi wenzetu wanavyoamka siku baada ya siku katika ndoto mbaya lakini bado wanaendelea na kutoa huduma zao kwa Wapalestina wanaowahitaji zaidi?"

Amesisitiza kuwa wafanyakazi wenzake wa Shirika hilo wanaendelea kutekeleza majukumu yao chini ya hali mbaya iliyopo Gaza, na huku UNRWA ikijitahidi kutekeleza majukumu yake katika hali inayozidi kuwa ngumu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Jerusalem Mashariki, Jordan, Lebanon na Syria, ili kupata maendeleo ya binadamu na utekelezaji wa haki za binadamu.

"Wito wangu kwa kila mtu ni huu lilinde UNRWA, linda wafanyakazi wa UNRWA, linda mamlaka ya UNRWA ikiwa ni pamoja na kupitia ufadhili," amesema.

Kwa kumalizia, amehimiza hatua kuanza bila kusubiri, kufanya kazi ya "kuweka matumaini mahali ambapo hakuna matumaini na kufanya kazi ili kuzingatia mamlaka ya Baraza Kuu kuilinda UNRWA."

Kamishna Jenerali wa UNRWA Philippe Lazzarini akiwa na wajumbe katika mshikamano wa vyombo mbele ya waandishi wa habari katika Baraza la Usalama.
UN News
Kamishna Jenerali wa UNRWA Philippe Lazzarini akiwa na wajumbe katika mshikamano wa vyombo mbele ya waandishi wa habari katika Baraza la Usalama.

UNRWA ukingoni kuporomoka kifedha

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Dennis Francis, ameonya kwamba "inapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kwetu kwamba UNRWA kwa sasa iko kwenye ukingo wa kuporomoka  kifedha, kutokana na huduma muhimu zinazotolewa na Shirika hilo na wafanyakazi wake."

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1949, UNRWA imejumuisha "kazi bora zaidi ya mashinani kwa miongo kadhaa, na kupata sifa kama mwanga wa matumaini katika eneo lenye matatizo ya mara kwa mara," amesema.

Amekumbusha kuwa shirika hilo linatoa ulinzi kwa wakimbizi milioni 5.9 waliosajiliwa, wakiwemo makundi hatarishi kama vile wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, na kwamba linasimamia kambi 58 zinazotambulika za Wapalestina, na kukidhi mahitaji ya dharura ya kibinadamu ya zaidi ya watu milioni 1.6 kote Jordan, Lebanon, Syria, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, pamoja na Jerusalem Mashariki.

Mgogoro unaoikabili UNRWA umezidishwa na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya sifa na uadilifu wake.

Francis amesema kwamba katika nyakati hizi ngumu wakati uwepo wa UNRWA uko hatarini, "tunapaswa kutambua kwamba mkutano huu wa ahadi hauwezi kuendelea kwa misingi ya biashara kama kawaida. Kwa hiyo ninahutubia hadhira ya kimataifa moja kwa moja, sasa, kuliko wakati mwingine wowote, UNRWA inahitaji msaada wako."

Familia huko Gaza zinaendelea kulazimishwa kusaka makazi katika maeneo salama.
© UNRWA
Familia huko Gaza zinaendelea kulazimishwa kusaka makazi katika maeneo salama.

Utaratibu wa kuishi

Kabla ya kumaliza taarifa yake, Rais wa Baraza Kuu alitoa wito wa kimya cha dakika moja ili kuenzi kumbukumbu ya wafanyakazi wenzake wa UNRWA waliopoteza maisha.

Francis amesisitiza wito wa kusitisha mapigano mara moja na wa kudumu kwa misingi ya kibinadamu huko Gaza, kufuata kwa pande zote sheria za kimataifa, kuwezesha upatikanaji wa haraka wa fursa  za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya Israeli kwa wahusika wa kibinadamu, na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.

Akihutubia Nchi Wanachama na wadau wengine wote ikiwa ni pamoja na mashirika ya misaada, sekta binafsi na watu binafsi, Francis amesema: "Sio tu kuhusu ufadhili, sio tu juu ya maisha ya shirika. Inahusu watu na maisha ya wakimbizi wa Palestina haswa watoto kote Ukanda wa Gaza, Jordan, Lebanon, Syria, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki."