Tinini (kundinyota)
Tinini (kwa Kilatini na Kiingereza Draco) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu.
Jina
Tinini ni jina lililotumiwa tangu zamani na mabaharia Waswahili waliojua njia yao baharini wakati wa usiku wakiangalia nyota[2]. Jina hili waliwahi kupokea kutoka Waarabu walioiita التنين at-tinniin na hili ni tafsiri ya Kigiriki Δράκων drakon (Draco kwa tahajia ya Kilatini).
Draco ilikuwa moja ya makundinyota 48 yaliyoorodheshwa na Klaudio Ptolemaio. Ilipokelewa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia katika orodha ya makundinyota 88 ya kisasa iliyotolewa mwaka 1930. [3] Kifupi rasmi ni ‘Dra’.[4]
Katika mitholojia ya Ulaya na Mashariki ya Kati Tinini au dragoni ni mnyama mkubwa mwenye umbo kama nyoka au mjusi, akiwa na miguu minne na mabawa mawili anayeweza kutema moto. Katika mitholojia ya Kigiriki ni Herakles alipambana pia na dragoni. Kundinyota Rakisi linalolingana na lile ya kumkumbuka Herakles (lat. Hercules) liko jirani na Tinini (Draco).
Mahali pake
Tinini - Draco iko katika karibu na ncha ya anga ya kaskazini, hivyo inaonekana kisehemu tu katika Afrika ya Mashariki na sehemu za nyota zake huwa chini ya upeo wa macho.
Inapaka na makundinyota jirani ya Dubu Mdogo (Ursa Minor), Dubu Mkubwa (Ursa Major), Bakari (Bootes), Rakisi (Hercules), Kinubi (Lyra), Dajaja (Cygnus) na Kifausi (Cepheus).
Nyota
Tinini - Draco ni kundinyota kubwa lenye nyota nyingi.
γ Gamma Draconis au “Etanin" ni nyota angavu zaidi. Ina mwangaza unaoonekana wa 2.2 ikuwa na umbali unaokadiriwa kuwa miakanuru 148[5]. Mwendo wake katika anga-nje unaelekea kwetu na katika miaka milioni 1.5 itakaribia hadi umbali wa miakanuru 28 na kuwa nyota angavu kabisa angani[6].
Jina la (Bayer) |
Namba ya Flamsteed |
Jina (Ukia) |
Mwangaza unaoonekana |
Umbali (miakanuru) |
Aina ya spektra |
---|---|---|---|---|---|
γ | 33 | Etamin au Eltanin | 2,23m | 150 | K5 III |
η | 14 | Aldhibain, Al Dhibain | 2,74m | 80 | G8 III |
β | 23 | Alwaid | 2,79m | 400 | G2 II |
δ | 57 | Altais | 3,07m | 100 | G9 III |
ζ | 22 | Aldhibah | 3,17m | 300 | B6 III |
ι | 12 | Edasich | 3,29m | 102 | K2 III |
χ | 44 | 3,57m | 25 | F7 V | |
α | 11 | Thuban | 3,65m | 300 | A0 III |
ξ | 32 | Grumium | 3,7m | ca. 110 | K2 III |
ε | 63 | Tyl | 3,83m | 147 | G7 + K5 |
λ | 1 | Gianfar | 3,8m | ca. 330 | M0 III |
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Draco" katika lugha ya Kilatini ni "Draconis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Draconis, nk.
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ "The IAU list of the 88 constellations and their abbreviations" ya mwaka 1922, kwenye tovuti ya Ian Ridpath, iliangaliwa Mei 2017
- ↑ Draco, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ Eltanin (Alfa Draconis), Tovuti ya Prof. Jim Kaler
Viungo vya Nje
- Constellation Guide: Draco constellation
- Draco, "Stars", kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
- Star Tales – Draco, tovuti ya Ian Ridpath, iliangaliwa Oktoba 2017
- The Deep Photographic Guide to the Constellations: Draco
Marejeo
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 202 ff (online hapa kwenye archive.org)
- Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331