WHO yatoa mwongozo wa kudhibiti uchafuzi unaosababishwa na watengenezaji wa viuavijasumu
WHO yatoa mwongozo wa kudhibiti uchafuzi unaosababishwa na watengenezaji wa viuavijasumu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limechapisha mwongozo wake wa kwanza kabisa kuhusu uchafuzi wa viuavijasumu unaotokana na uzalishaji viwandani. Mwongozo huu unaohusu usimamizi wa maji taka na taka ngumu katika uzalishaji wa viuavijasumu unaangazia changamoto hii iliyopuuzwa huku dunia ikisubiri Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kuhusu vijidudu au vijiumbe maradhi vyenye usugu kwa dawa za viua vijiumbe maradhi, au AMR unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Septemba 2024
Katika taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari leo, Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Yukiko Nakatani, amesema "taka za dawa kutoka kwenye uzalishaji wa viuavijasumu zinaweza kusababisha kuibuka kwa bakteria wapya wenye usugu kwa dawa, ambao wanaweza kuenea duniani kote na kutishia afya yetu. Kudhibiti uchafuzi kutoka kwenye uzalishaji wa viuavijasumu kunachangia katika kuhifadhi ufanisi wa dawa hizi za kuokoa maisha kwa kila mtu."
Mwongozo huu wa WHO pia umebainisha kuwa kuibuka na kuenea kwa AMR kunakosababishwa na uchafuzi wa viuavijasumu kunaweza kudhoofisha ufanisi wa viuavijasumu kote duniani, ikiwemo dawa zinazozalishwa katika maeneo ya uzalishaji yanayohusika na uchafuzi huo.
Hata hivyo, licha ya ripoti nyingi kuhusu viwango vya juu vya uchafuzi wa viuavijasumu, suala hili halijadhibitiwa ipasavyo na vigezo vya uhakikisho wa ubora havishughulikii utoaji wa uchafuzi wa mazingira. Aidha, mara baada ya kusambazwa, kuna ukosefu wa taarifa zinazotolewa kwa watumiaji kuhusu jinsi ya kutupa viuavijasumu wanapokuwa hawajavitumia, kwa mfano, vinapokwisha muda wake au wanapomaliza vipimo lakini bado kuna mabaki ya dawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Afya WHO, Dk. Maria Neira, amesema "duniani kote, kuna upungufu wa taarifa zinazopatikana kuhusu uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uzalishaji wa dawa. Mwongozo huu unatoa msingi wa kisayansi ulio huru na usioegemea upande wowote kwa ajili ya wasimamizi, wanunuzi, wakaguzi, na sekta yenyewe kujumuisha udhibiti thabiti wa uchafuzi wa viuavijasumu katika viwango vyao. Muhimu zaidi, mkazo mkubwa uliowekwa kwenye uwazi utawawezesha wanunuzi, wawekezaji na umma kwa ujumla kufanya maamuzi yanayozingatia juhudi za wazalishaji kudhibiti uchafuzi wa viuavijasumu."
Mkuu wa Kitengo cha Sekta na Uchumi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la la Mazingira (UNEP), Jacqueline Alvarez, alibainisha kwamba "nafasi ya mazingira katika maendeleo, usafirishaji, na kuenea kwa usugu wa vijiumbe maradhi dhidi ya dawa inahitaji kuzingatiwa kwa makini kwani ushahidi unaendelea kuongezeka. Kuna makubaliano ya pamoja kwamba hatua kuhusu mazingira lazima iwe na umuhimu zaidi kama suluhisho. Hii inajumuisha kuzuia na kudhibiti uchafuzi kutoka kwa mifumo ya manispaa, maeneo ya uzalishaji, vituo vya afya, na mifumo ya chakula na kilimo."
Mwongozo huu unatoa malengo yanayozingatia afya ya binadamu ili kupunguza hatari ya kuibuka na kuenea kwa AMR, pamoja na malengo ya kushughulikia hatari kwa viumbe vya majini inavyosababishwa na viuavijasumu vyote vinavyokusudiwa kwa matumizi ya binadamu, wanyama, au mimea.
AMR hutokea wakati bakteria, virusi, fangasi, na vimelea haviuliwi tena kwa dawa, hali ambayo huwafanya watu kuwa wagonjwa zaidi na kuongeza hatari ya kuenea kwa maambukizi ambayo ni magumu kutibu, magonjwa, na vifo.