Kanisa (jengo)
Kuhusu jumuiya ya Wakristo angalia makala Kanisa
Kanisa ni maabadi maalumu ya Wakristo. Hao, walipoanza kujenga mahali pa ibada, pakaja kuitwa kanisa kwa sababu ndani yake walikusanyika wao, Kanisa hai.
Hivyo hadi leo mara nyingi neno hilo linatumika kwa maana ya jengo. Mtume Paulo aliwahi kulinganisha umoja wa Wakristo na jengo aliloliita "nyumba ya Mungu", iliyojengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, huku akimfananisha Yesu na jiwe kuu la msingi[1].
Historia ya ujenzi wa makanisa
Wakristo wa kwanza walikutana katika nyumba za kawaida. Habari za majengo ya pekee kwa ajili ya ibada zilianza mara ya kwanza wakati wa karne ya 3.
Mnamo mwaka 260 Kaizari Galienus aliamuru kumaliza dhuluma dhidi ya Wakristo yaliyoanzishwa upya na Kaizari Valerian, baba yake, akaamuru pia kwamba mahali pa kuabudu parudishwe kwao. Pia katika karne ya 3 mwanafalsafa Porphyrus aliandika kwamba Wakristo wanajaribu kuiga mahekalu kwa kujenga nyumba kubwa.[2] Hatujui majengo hayo ya kwanza yalionekana vipi. Kuna mfano mmoja tu uliogunduliwa ambao ni kanisa la mjini Dura Europos (Syria) ambalo liliwahi kuwa nyumba ya binafsi iliyobadilishwa kuwa na chumba kikubwa cha ibada[3].
Baada ya mwaka 312 hali ya majengo ya Wakristo ilibadilika. Mwaka ule Ukristo ulitangazwa mara y akwanza kuwa dini halali katika Dola la Roma. Kaizari Konstantino I aliamini kwamba alimshinda mpinzani wake kwa msaada wa Mungu wa Wakristo akajitolea kuagiza ujenzi wa makanisa makubwa kwamba vile Kanisa kuu la Roma katika mtaa wa Laterani lililoendelea kuwa kanisa kuu la askofu wa Roma hadi leo, kanisa juu ya kaburi la Yesu mjini Yerusalemu, kanisa juu ya pango ambako Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, pamoja na makanisa mengine. Konstantino aliagiza pia magavana wake kugharamia ukarabati wa makanisa yaliyochakaa au kuharibika katika dhuluma dhidi ya Wakristo zilizotangulia. Pia makaizari waliofuata waliagiza ujenzi wa makanisa na mfano mashuhuri zaidi ni Hagia Sophia mjini Konstantinopoli iliyojengwa kwa amri ya Kaizari Justiniani I.
Katika karne zilizofuata ujenzi wa makanisa uliendelea kulingana na utamaduni wa nchi mbalimbali na uwezo wa jumuiya ya wajenzi.
Mitindo ya ujenzi
Makanisa hayo makubwa baada ya Konstantino yalifuata mtindo wa mabasilika ambayo yalikuwa kumbi kubwa zenye umbo la mstatili katika miji ya Kiroma zilizotumiwa kama ukumbi wa mahakama au wa soko. Upande mfupi mmojawapo wa mstatili ulikuwa na kishubaka cha kiduara ambako sanamu ya mtawala ilisimama, pamoja na kiti cha jaji kwenye jengo la mahakama.
Makanisa yaliyofuata mtindo wa basilika hupanua ukumbi kwa msaada wa mistari miwili au zaidi ya nguzo zinazogawa ukumbi wote katika sehemu kuu na sehemu za pembeni. Juu ya sehemu kuu ya katikati ukumbi huwa na kimo kikubwa kuliko sehemu za pembeni. Sehemu ya kishubaka sasa ni mahali pa altare.
Katika Ulaya ya magharibi, basilika liliendelea kupata umbo la msalaba katika enzi ya kati.
Tangu siku za mabasilika, makanisa mengi yalielekezwa kutoka magharibi yakitazama altare upande wa mashariki.
Makanisa ya pekee yalijengwa kwa ajili ya ibada za ubatizo, mara nyingi yenye umbo la duara. Hilo limekuwa umbo linalotumiwa mara nyingi kwa makanisa nchini Ethiopia.
Kuna pia makanisa mengine yasiyotumia umbo la mstatili, nje ya umbo la duara kuna pia umbo la mraba au umbo la msalaba wenye mikono sawa.
Katika utamaduni wa Ulaya, kuanzia karne ya 12 katika Mtindo wa Kigothi wajenzi walijifunza kutumia gadi za nje ya ukuta zilizobeba uzito wake na hivyo waliweza kuwa na madirisha makubwa yanayoingiza mwanga mwingi ndani ya kanisa.
Majengo hayo ya ibada yanaweza kuwa na ubora tofauti hata upande wa sanaa; baadhi yake yanatembelewa na watalii na kuhifadhiwa kwa bidii kwa sababu hiyo.
Kwa namna ya pekee ni muhimu Kanisa kuu la kila jimbo, halafu Basilika na Patakatifu, lakini pia kanisa la parokia, kanisa la kigango[4]
Marejeo
- ↑ Waraka kwa Waefeso 2,20
- ↑ Porphyry, [https://www.tertullian.org/fathers/porphyry_against_christians_02_fragments.htm Against the Christians] (2004). Fragments. (kifungu 76. Macarius, Apocriticus IV: 21: )
- ↑ Hopkins, Clark (1934). "The Christian Church". The Excavations At Dura Europos. pp. 238–288. Retrieved 20 December 2021.
- ↑ Hilo pengine linaitwa sunagogi, ambalo kwa kweli ni jina la majengo ya Wayahudi.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kanisa (jengo) kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |