Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki
Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki (Kiing. East African Rift Valley) ni maumbile ya kijiolojia yanayoanza katika Mashariki ya Kati na kuendelea hadi Msumbiji. Ni kati ya maajabu makubwa ya dunia. Ufa huu ulitengenezwa miaka milioni 25 iliyopita kutokana na mwendo wa mabamba ya gandunia ya Afrika na Uarabuni.[1] Mwendo huu umesababisha pia farakano ndani ya bamba la Afrika na wataalamu huamini kuwa Afrika ya Mashariki iko katika mwendo wa kuachana na Afrika kwa jumla.[2]
Ueneaji
[hariri | hariri chanzo]Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki lina urefu wa kilomita 6,000 kuanzia chanzo chake katika Jordan hadi mwisho wake upande wa kusini katika Msumbiji. Upana wake ni kati ya kilomita 30 na zaidi ya 100; kina chake ni kati ya mita mia kadhaa hadi maelfu.
Sehemu ya Asia ya Magharibi
[hariri | hariri chanzo]Upande wa kaskazini ufa unaanza kwenye mpaka wa Syria na Lebanoni ukionekana katika uwanja wa Beka'a kati ya milima ya Lebanoni na milima ya Lebanoni ndogo.
Bonde hilo linaendelea katika mabonde ya mto Yordani na Wadi Araba hadi kuingia katika Ghuba ya Akaba na Bahari ya Shamu.[3]
Sehemu ya Uhabeshi
[hariri | hariri chanzo]Ufa unaonekana tena upande wa Afrika kwenye Pembetatu ya Afar mpakani mwa Eritrea, Jibuti na Ethiopia. Hapa ufa umegawanyika. Mkono moja unaelekea mashariki-kaskazini katika Ghuba ya Aden.
Mkono mkuu umepasua nyanda za juu za Ethiopia na nyanda za juu za Somalia ukielekea kusini. Mto Awash unafuata sehemu ya kaskazini ya bonde hili. Katika sehemu ya kusini kuna maziwa kama ziwa Abaya.[4]
Kugawanyika katika Kenya
[hariri | hariri chanzo]Mpakani mwa Ethiopia na Kenya, bonde la ufa lajigawa kuwa na mikono miwili.
Mkono wa mashariki
[hariri | hariri chanzo]Mkono wa mashariki unaonekana katika ziwa Turkana na kuelekea kusini. Karibu na Nairobi unatokea kama bonde kubwa lenye kina kikubwa. Maziwa mengine ni maziwa kama Baringo, Bogoria, Elementaita, Nakuru na Naivasha.
Mpakani na Tanzania kuna maziwa ya magadi kama Ziwa Natron. Ndani ya Tanzania baada ya kupita mlima Kilimanjaro bonde lapanuka hadi kutotambulika tena kwa macho. Kwenye uwanja wa Usangu linaonekana tena kama bonde lenye safu za milima kando. Mjini Mbeya mkono huu unakutana tena na mkono wa mashariki na kuendelea pamoja katika ziwa Nyasa.[5]
Mkono wa magharibi
[hariri | hariri chanzo]Mkono wa magharibi huonekana vizuri kuanzia ziwa Albert na kuendelea katika maziwa ya Edward, Kivu, Tanganyika na Rukwa. Mbeya unakutana na mkono wa mashariki.
Kando ya ufa kuna milima ya juu yenye asili ya kivolkeno kama vile safu za Virunga, Mitumba na Ruwenzori.
Sehemu ya Kusini
[hariri | hariri chanzo]Kusini mwa Mbeya ufa unaendelea katika Ziwa Nyasa halafu katika mabonde ya mto Shire na sehemu ya mwisho wa mto Zambezi hadi kuingia katika Bahari ya Hindi.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://academic.oup.com/astrogeo/article/46/2/2.16/216710
- ↑ https://timesofindia.indiatimes.com/travel/destinations/africa-is-slowly-breaking-into-two-continents/as69465241.cms#:~:text=The%20continent%20of%20Africa%20is,the%20side%20of%20the%20continent.&text=The%20East%20African%20Rift%20Valley,Gulf%20of%20Aden%20to%20Zimbabwe.
- ↑ https://www.britannica.com/place/East-African-Rift-System
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-10-19. Iliwekwa mnamo 2021-07-23.
- ↑ https://www.geolsoc.org.uk/Policy-and-Media/Outreach/Plate-Tectonic-Stories/Vale-of-Eden/East-African-Rift-Valley
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Geographical description
- Small simple-coloured map Ilihifadhiwa 20 Septemba 2009 kwenye Wayback Machine.
- Maps from the Albertine Rift Programme Ilihifadhiwa 26 Oktoba 2005 kwenye Wayback Machine.