Nenda kwa yaliyomo

Historia ya teolojia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
The printable version is no longer supported and may have rendering errors. Please update your browser bookmarks and please use the default browser print function instead.
Filo wa Aleksandria

Historia ya teolojia inapitia mchango wa wataalamu mbalimbali katika kuchunguza Mungu ni nani pamoja na kazi yake.

Ugiriki wa Kale

Falsafa ilijaribu mapema kukabili suala la Mungu na miungu. Kati ya waliofanya kwanza kazi hiyo kuna Hesiodo (maandishi ya mwaka 700 KK hivi), Sokrate (470 KK hivi - 399 KK), Plato (maandishi ya mwaka 360 KK) na Aristotle (maandishi ya mwaka 330 KK)

Walioendelea ni kama vile: Cleanthes (karne ya 3 KK), Cicero (maandishi ya mwaka 45 KK), Lucretius (karne ya 1 KK), Epictetus (maandishi ya mwaka 135) na Plotinus (kuanzia 235). Baadhi ya hawa walikuwa Walatini walioathiriwa na ustaarabu wa Kigiriki.

Wakati huohuo falsafa ilianza kuathiriwa na dini iliyomuabudu Mungu mmoja, hususan Uyahudi na Ukristo.

Uyahudi

Katika karne ya 1 na ya 2 BK, dini ya Kiyahudi upande mmoja ilijiimarisha katika utaalamu wa Tanakh (Biblia ya Kiebrania), upande mwingine ilijadiliana na falsafa ya Kigiriki hasa nchini Misri, kulikokuwa na mji wa Aleksandria, makao makuu ya elimu wakati huo: ndipo alipojitokeza hasa Filo (20 KK - 40 BK).

Ukristo

Maandishi ya Agano Jipya ya Biblia ya Kikristo (karne ya 1) hayaishii katika kusimulia habari za Yesu (6 KK - 30 BK hivi) na mafundisho yake, bali yanaleta tafakuri za dhati juu ya imani hiyo mpya, hasa katika nyaraka za Mtume Paulo (6 - 67 hivi) na vitabu vya Mtume Yohane (10 - 100 hivi).

Kadiri Ukristo ulivyozidi kuenea hata kati ya wasomi, teolojia ilihitajika ili kuchambua ukweli wa matamko ya waumini, kwa kukataa uzushi. Katika kazi hiyo walijitokeza hasa mababu wa Kanisa, wanaume maarufu kwa elimu, imani sahihi, utakatifu pamoja na ukale (yaani kuishi katika karne za kwanza za Kanisa).

Kati ya wale wa kwanza, kuna Yustino mfiadini (100/114162/168), Ireneo wa Lyons (130 hivi – 202) na Klementi wa Aleksandria (hadi 215).

Baadaye Tertuliani (155 hivi - 230 hivi), Hipoliti wa Roma (hadi 235), Origen (182 hivi - 251 hivi), Sipriani mfiadini (hadi 258). Mzushi aliyefuatwa na wengi zaidi wakati huo ni Arios (256-336).

Askofu Agostino wa Hippo.

Baada ya Mtaguso wa kwanza wa Nisea (325) kufikia uamuzi muhimu kuhusu mabishano yaliyotangulia, walizidi kujitokeza wanateolojia bora: Atanasi wa Aleksandria (298-373), Mababu wa Kapadokia (hasa Basili Mkuu, Gregori wa Nazianzo na Gregori wa Nisa mwishoni mwa karne ya 4), Ambrosi (340 hivi -397), Yohane Krisostomo (347-407), Jeromu (347 hivi - 420), Agostino wa Hippo (354-430), Sirili wa Aleksandria (376-444), Leo Mkuu (400 hivi - 461) na Gregori Mkuu (540 hivi - 604).

Baada ya kipindi cha mababu kama hao kwisha, Ukristo wa Mashariki na Ukristo wa Magharibi vilizidi kuelekea tofauti katika teolojia na mengineyo, na hatimaye umoja kuvunjika vibaya hasa mwaka 1054.

Martin Luther.

Tofauti kubwa zaidi zilijitokeza magharibi kuanzia matengenezo ya Kiprotestanti (karne ya 16). Jibu lilitolewa hasa na urekebisho wa Kikatoliki na Mtaguso wa Trento.

Kuanzia karne ya 20, juhudi za ekumeni zimeelekea kurudisha umoja wa imani kwa kujadiliana na kukwepa mabishano ya bure.

Uislamu

Teolojia ya Uislamu ilijitokeza mwishoni mwa karne ya 7 kuhusu suala la uhusiano kati ya Maongozi ya Mungu na hiari ya binadamu (mabishano kati ya Qadariyyah na Jabriyyah).

Baadaye (karne ya 9) ilijitokeza pia falsafa ya Kiislamu

Tanbihi

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.