Krismasi
Krismasi (pia Noeli) ni sikukuu ambayo Wakristo wengi husheherekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.
Kwa kawaida husheherekewa tarehe 25 Desemba katika Ukristo wa magharibi[1] na tarehe 6 Januari katika ule wa mashariki.
Jina
Kwa Kiswahili kuna majina mawili ya kawaida kwa ajili ya sikukuu hii:
- Krismasi kutokana na neno la Kiingereza lenye maana ya "Christ`s Mass" yaani misa au ibada ya Kristo.
Historia ya sherehe ya Krismasi
Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Hakuna uhakika kamili ni lini Krismasi ilianza kusheherekewa. Ni sikukuu ya kale katika Ukristo lakini haikuwepo tangu mwanzoni. Tarehe halisi ya kuzaliwa kwake Yesu haijulikani kwa sababu utamaduni wa Wayahudi wa wakati ule haukuwa na sherehe au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa.
Lakini baadaye Ukristo ulienea katika Dola la Roma kati ya mataifa yaliyokuwa na kawaida ya kuzingatia siku ya kuzaliwa. Hivyo ilijitokeza hamu ya kusheherekea pia sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Ndiyo asili ya sikukuu ya Krismasi.
Tangu mwanzo wa karne ya 3 BK kuna kumbukumbu ya waandishi mbalimbali waliojadili tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
Habari za kwanza kabisa za makadirio ya tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu zinapatikana kutoka Misri mnamo mwaka 200 BK. Mwandishi Mkristo Klemens wa Alexandria [2] alilalamikia udadisi wa wataalamu kadhaa wa Misri waliodai kwamba wamekadiria tarehe hiyo katika mwezi Mei, wengine katika Aprili. Alisema pia kuwa kikundi cha Kikristo cha wafuasi wa Basilides huko Misri walisheherekea Epifania pamoja na kuzaliwa kwake Yesu tarehe 6 Januari.
Lakini kadirio la tarehe 25 Desemba lina asili katika Misri pia. Kuanzia mwaka 200 (kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Sixtus Julius Africanus) wataalamu nchini Misri waliona tarehe 14 Nisan ya kalenda ya Kiyahudi ambayo ni sawa na 25 Machi ilikuwa tarehe ya kufa kwake Kristo na pia siku ya utungaji mimba wake. Kwa kuongeza miezi tisa ya mimba inajitokeza 25 Desemba kama tarehe ya kuzaliwa.
Inaonekana tarehe 25 Desemba ilijitokeza wakati huo. Kuna taarifa ya mwaka 204 kutoka Ipolito wa Roma kwamba tarehe 25 Desemba ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
Krismasi na sikukuu ya Sol Invictus
Mjini Roma wakati wa karne ya 4 tarehe ya Krismasi katika Desemba ilitokea pamoja na sikukuu ya Kipagani iliyoitwa "Siku ya Sol Invictus". Hii ilikuwa sherehe ya Jua kama mungu "Sol invictus" (yaani "Jua lisiloshindika"). Hii ilikuwa ibada iliyoingia Roma kutoka Uajemi ambako mungu Mithra aliabudiwa kama mungu wa nuru.
Waumini wa dini ya Jua waliona wakati wa Desemba kama kipindi cha pekee kutokana na solistasi ya mwezi huo; katika nusutufe ya kaskazini ya Dunia urefu wa mchana unapungua na usiku unakuwa mrefu tangu sikusare ya 21/22 Septemba hadi tarehe 21/22 Desemba; kuanzia siku za 21/22 Desemba mchana huwa mrefu na nuru inaongezeka. Mwendo huo ulitazamwa kama ushindi wa nuru = Jua juu ya giza.
Pale Roma Kaisari Eliogabalus (aliyezaliwa Syria, alitawala Roma 218 hadi 222) alianzisha sherehe ya sikukuu ya "Kuzaliwa Jua" huko Roma. Baadaye Kaisari Aurelianus akaithibitisha rasmi mwaka 273.
Wakati wa Kaisari Licinius (308-324) sikukuu hiyo ilikuwa ikiadhimishwa bado tarehe 19 Desemba. [3]. Hatimaye ikahamishiwa tarehe 25 Desemba.
Wataalamu mbalimbali walidai kwamba Kanisa lilipachika sikukuu ya Kristo kwenye tarehe hiyo kwa nia ya kufanya ichukue nafasi ya sikukuu ya jua kama mungu "Sol invictus" (yaani "Jua lisiloshindika"). Kwa namna yoyote hata katika Ukristo Jua linatazamwa kama ishara ya Kristo; katika sehemu mbalimbali za Biblia Kristo alifananishwa tayari na Jua na maneno haya yaliandikwa muda mrefu kabla ya kutokea kwa siku ya Sol Invictus. Mifano ni Injili ya Luka 1,78 [4]Ufunuo 21, 23 [5], Malaki 4,2 ([6], hivyo katika mashindano na dini ya kuabudu Jua Wakristo walitumia lugha ya Biblia kwa kudokeza Kristo ndiye Jua la kweli.
Kutoka Roma, uliokuwa mji mkuu wa Dola la Roma, sherehe ya 25 Desemba ilienea kote katika Ukristo.
Wakristo wengi husheherekea tarehe 25 Desemba (Wakatoliki na sehemu ya Waprotestanti na Waorthodoksi). Kati ya Waorthodoksi kuna tarehe nyingine, hasa 6 Januari kutokana na tofauti katika kalenda.
Habari za Krismasi katika Biblia
Habari za Krismasi kama sherehe hazipatikani katika Biblia kwa sababu zilizotajwa hapa juu na kwa sababu mwanzoni mwa Kanisa mkazo ulikuwa juu ya kifo na ufufuko wa Yesu, tunavyoona hasa katika barua za Mtume Paulo.
Baadaye tu, Wakristo walichunguza zaidi asili ya huyo aliyesadikiwa nao kuwa alikufa na kufufuka.
Hasa vitabu viwili vya Agano Jipya vina habari za kuzaliwa kwake Yesu, yaani Injili za Mathayo na Luka.
Katika Injili ya Mathayo
Mathayo anasimulia habari hizo katika mlango wa kwanza kuanzia aya 18[7] na katika mlango wa pili[8].
Bikira Maria, Mama wa Yesu, alipata mimba wakati alipokuwa mchumba wa Yosefu. Yosefu alitaka kumwacha lakini aliambiwa na malaika aanze kuishi naye na kumkubali mtoto kama wake kwa kumpa jina "Yesu".
Mamajusi kutoka mashariki waliwatembelea kijijini Bethlehemu na kuwaletea zawadi kwa sababu waliona nyota ya pekee iliyokuwa kwao alama ya kuzaliwa kwa mfalme mpya katika Uyahudi ikawaongoza hadi mjini Yerusalemu. Lakini walipompitia mfalme Herode Mkuu, huyo alikasirika akimwogopa mfalme mpya. Hata hivyo aliwaelekeza Bethlehemu kadiri ya utabiri wa nabii Mika.
Yosefu alipata tena ujumbe kutoka kwa malaika akaondoka na mtoto na Maria kukimbilia Misri kabla ya askari wa Herode hawajaweza kumuua Yesu.
Baada ya kifo cha Herode walirudi kutoka Misri lakini hawakuenda tena Bethlehemu bali walihamia Nazareti katika mkoa wa Galilaya.
Katika Injili ya Luka
Katika taarifa ya Luka (mlango wa 1 na 2) Maria alipokea huko Nazareti ujumbe wa malaika mkuu Gabrieli kwamba atapata mimba halafu mtoto wa pekee.[9]
Yosefu na Maria walikwenda Bethlehemu kwa sababu ya sensa iliyowataka kwenda katika mji asili wa ukoo wa Yosefu, mjukuu wa mfalme Daudi. Hapo Yesu alizaliwa katika hori la kulishia wanyama; wachungaji mabondeni walitangaziwa na malaika habari hiyo wakaja kumwona mtoto.[10]
Baada ya kuzaliwa wazazi walimpeleka Yesu Yerusalemu katika hekalu kufuatana na sheria ya Agano la Kale (Kitabu cha Kutoka 13,2; 13,15) halafu wakarudi kwao Nazareti.[11]
Habari za Krismasi katika Korani
Korani pia ina habari za kuzaliwa kwake Yesu (nabii Isa).
Sura ya tatu (Al Imran, 42-47) ina habari za tangazo la malaika kwa Bikira Mariamu zinazofanana na Luka 1.
Sura ya 19 (Mariamu, 16-34) inarudia tangazo la malaika kwa Mariamu na inasimulia kuzaliwa kwake Yesu chini ya mti wa mtende, halafu majadiliano kati ya Mariamu na ndugu zake. Mtoto mchanga Yesu akaanza kusema wakati wa kuzaliwa akimtetea mama yake dhidi ya ndugu zake.
Krismasi katika liturujia
Kama kawaida, imani na liturujia ya Kikristo zinaitikia haja za binadamu.
Mojawapo ni kukutana na watu wa kupendeza kwa wema wao.
Kipindi cha Noeli kinatimiza haja hiyo, kwa kuwa kinaadhimisha kuzaliwa kwa mtu mpya kabisa ambaye anatuvutia kwa wema wake na ambaye tukimuona tumemuona Mungu, tena tukimpokea tunazaliwa upya kama wana wa Mungu.
“Leo amezaliwa kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana”. Tunapoadhimisha Noeli tangazo hilo la malaika kwa wachungaji linatufikia sisi. Si kujidanganya, kana kwamba Yesu angezaliwa leo, wala hatukumbuki tu tukio la zamani, bali fumbo la kuzaliwa Bwana linatufikia leo katika liturujia na kutuletea neema zake. Hivyo tunaweza tukazaliwa upya kwa kushiriki kuzaliwa kwa kichwa chetu.
Liturujia inashangilia hivi, “Lo! Mabadilishano ya ajabu! Mwana wa Mungu anakuwa mtu kusudi mtu awe mwana wa Mungu!”. Tena si binadamu tu, bali viumbe vyote vinapata heshima mpya kwa Neno wa milele kujifanya kiumbe.
Desturi za Krismasi
Sherehe ya Krismasi imekuwa sikukuu muhimu sana katika tamaduni za mataifa yaliyoathiriwa na Ukristo. Kuna desturi nyingi zilizojitokeza katika karne zote za kusheherekea Krismasi. Sehemu ya desturi hizi zimeenea pia nje ya nchi za asili na hata kutumiwa na watu wasiofuata imani ya Kikristo.
- Pango la Noeli lililoanzishwa na Fransisko wa Asizi mwaka 1223 kijijini Greccio (Italia ya Kati) na kuenea kila mahali kama sanaa inayoonyesha kwa njia mbalimbali jinsi Yesu alivyozaliwa.
- Mapambo ya Krismasi: ni hasa nuru na taa za pekee. Alama za nyota kwa kukumbuka nyota iliyopeleka mamajusi hadi Bethlehemu inawekwa ndani na nje ya nyumba na maduka.
- Mti wa Krismasi - ni ishara ya pekee ya Krismasi yenye asili katika Ujerumani kusini-magharibi ya karne ya 16 hivi. Asili yake iko katika maigizo yaliyosimulia hadithi za Biblia na mti wa Paradiso unaohusiana na masimulizi ya dhambi la kwanza na ujumbe wa Kristo kama mwokozi anayekuja kuondoa dhambi hilo. Kutoka maigizo ya kanisani ishara ya mti uliopambwa matunda uliingia katika nyumba za Wakristo ambako ulipambwa zaidi kwa matunda, keki tamu na pipi kwa watoto. Umekuwa mapambo ya nyumbani kwa majira ya Krismasi. Tangu Krismasi kuwa nafasi muhimu kwa uchumi kuna pia maduka mengi yanayoweka miti hii na katika mazingira ya kibiashara uhusiano wake na mti wa Paradiso umesahauliwa mara nyingi.
- Zawadi za Krismasi - Martin Luther alitaka kuongeza umuhimu wa Krismasi kwa Wakristo ambao wakati wake walikuwa na desturi ya kuwazawadia watoto kwenye siku ya Mtakatifu Nikolasi tarehe 6 Desemba, wiki 2 kabla ya sikukuu. Hapo Luther alipendekeza kuhamisha zawadi kwa watoto kwenda siku ya kuzaliwa kwake Yesu ili wamkumbuke zaidi Yesu kuliko mtakatifu huyo. Hapo alirejea zawadi zilizopelekwa kwa Yesu na mamajusi kutoka mashariki kufuatana na taarifa ya Injili ya Mathayo mlango 2. Desturi ya kuwazawadia watoto kwenye sikukuu hii ilienea hadi kuwa desturi ya kupeana zawadi kati ya watu wa kila umri. Katika karne ya 20 desturi ilienea kiasi cha kuwa nafasi muhimu ya biashara. Katika nchi nyingi mwezi Desemba umekuwa mwezi wa mapato makubwa kushinda miezi mingine. Hata katika miji mikubwa ya nchi kama Dubai au Japani ambako Wakristo ni wachache desturi ya kupeana zawadi imeenea na mapambo ya Krismasi katika maduka yanataka kuwahamasisha wateja kununua zawadi za majira.
Tanbihi
- ↑ Martyrologium Romanum
- ↑ (kitabu cha Stromateis I, xxi)
- ↑ Taz. maandishi yaliyotajwa na Allan S. Hoey katika ukurasa 480 (rejeo 128) wa Official Policy towards Oriental Cults in the Roman Army, Transactions and Proceedings of the American Philological Association (70) 1939, pp 456-481)
- ↑ Nuru ya jua itatujia kutoka mbinguni na kuwaangazia wote
- ↑ Mwanakondoo ataangaza Yerusalemu badala ya Jua
- ↑ "kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia", maneno yaliyosomwa na Wakristo kama utabiri wa kuja kwa Kristo
- ↑ 1:18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19 Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. 20 Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21 Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao." 22 Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: 23 "Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi"). 24 Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. 25 Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.
- ↑ 2:1 Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, 2 wakauliza, "Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu." 3 Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. 4 Basi akawaita pamoja makuhani wakuu wote na walimu wa Sheria, akawauliza, "Kristo atazaliwa wapi?" 5 Nao wakamjibu, "Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: 6 `Ewe Bethlehemu katika nchi ya Yuda, kwa vyovyote wewe si mdogo kabisa kati ya viongozi wa Yuda; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli."` 7 Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. 8 Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, "Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende nikamwabudu." 9 Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. 10 Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. 11 Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani na manemane. 12 Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine. 13 Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokwambia, maana Herode anakusudia kumwua huyu mtoto." 14 Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. 15 Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: "Nilimwita Mwanangu kutoka Misri." 16 Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. 17 Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: 18 "Sauti imesikika mjini Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki." 19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20 akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa." 21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: "Ataitwa Mnazare."
- ↑ 1:26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34 Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35 Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37 Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38 Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
- ↑ 2:1 Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe. 2 Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. 3 Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake. 4 Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi. 5 Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito. 6 Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, 7 akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. 8 Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. 10 Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote. 11 Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. 12 Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini." 13 Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: 14 "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!" 15 Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha." 16 Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. 17 Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. 18 Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. 19 Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. 20 Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. 21 Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
- ↑ 2:22 Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana. 23 Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana." 24 Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana. 25 Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. 26 Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana. 27 Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria, 28 Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema: 29 "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani. 30 Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako, 31 ambao umeutayarisha mbele ya watu wote: 32 Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli." 33 Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. 34 Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; 35 na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako." 36 Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. 37 Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. 38 Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. 39 Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya. 40 Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye.
Marejeo
- Restad, Penne L. (1995). Christmas in America: A History. New York: Oxford University Press. ISBN 0-19-509300-3.
- The Battle for Christmas, by Stephen Nissenbaum (1996; New York: Vintage Books, 1997). ISBN 0-679-74038-4
- The Origins of Christmas, by Joseph F. Kelly (August 2004: Liturgical Press) ISBN 978-0-8146-2984-0
- Christmas Customs and Traditions, by Clement A. Miles (1976: Dover Publications) ISBN 978-0-486-23354-3
- The World Encyclopedia of Christmas, by Gerry Bowler (October 2004: McClelland & Stewart) ISBN 978-0-7710-1535-9
- Santa Claus: A Biography, by Gerry Bowler (November 2007: McClelland & Stewart) ISBN 978-0-7710-1668-4
- There Really Is a Santa Claus: The History of St. Nicholas & Christmas Holiday Traditions, by William J. Federer (December 2002: Amerisearch) ISBN 978-0-9653557-4-2
- St. Nicholas: A Closer Look at Christmas, by Jim Rosenthal (July 2006: Nelson Reference) ISBN 1-4185-0407-6
- Just say Noel: A History of Christmas from the Nativity to the Nineties, by David Comfort (November 1995: Fireside) ISBN 978-0-684-80057-8
- 4000 Years of Christmas: A Gift from the Ages, by Earl W. Count (November 1997: Ulysses Press) ISBN 978-1-56975-087-2
- Sammons, Peter (Mei 2006). The Birth of Christ. Glory to Glory Publications (UK). ISBN 0-9551790-1-7.
{{cite book}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)
Viungo vya nje
Angalia mengine kuhusu Krismasi kwenye miradi mingine ya Wikimedia: | |
Fafanuzi za Kiingereza kutoka Wiktionary | |
picha na media kutoka Commons | |
nukuu kutoka Wikiquote | |
matini za ushuhuda na vyanzo kutoka Wikisource | |
vitabu kutoka Wikibooks |
- Christmas katika Open Directory Project
- Christmas: Its Origin and Associations, by William Francis Dawson, 1902, from Project Gutenberg