Baada ya Kristo
Baada ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo (kifupi: BK) ni namna ya kutaja miaka ambayo imekuwa njia ya kuhesabu miaka inayotumika zaidi duniani.
Kila mwaka huhesabiwa kuanzia ule uliodhaniwa kuwa mwaka wa kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Miaka iliyotangulia kuzaliwa kwake Yesu huitwa Kabla ya Kuzaliwa kwake Yesu Kristo au kifupi: KK.
Historia ya hesabu "Kabla ya / Baada ya Kristo"
haririHesabu hii ilianzishwa mwaka 527 BK na mmonaki Dionysius Exiguus alipokuwa Roma.
Wakati ule mahesabu mbalimbali ya miaka yalikuwa kawaida. Mwaka uleule uliweza kuitwa kutokana na muda wa utawala wa Mfalme au Kaisari (kwa mfano: mwaka wa 5 wa Kaisari Iustiniano) na pia kuanzia tarehe ya kuundwa kwa mji wa Roma (kwa mfano: mwaka 1185 ab Urbe Condita = tangu kuanzishwa kwa mji).
Mahesabu mengine yaliyokuwa kawaida wakati ule ni makadirio mbalimbali "tangu kuumbwa kwa dunia" na mengineyo.
Dionysio baada ya kufanya utafiti alidhani Yesu alizaliwa mwaka 754 tangu kuanzishwa kwa Roma.
Hesabu yake haijui mwaka "0"; tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu huchukuliwa kama mwanzo wa mwaka. Kwa hiyo moja kwa moja inaingia katika mwaka "1" na mwaka kabla yake ni mwaka 1 kabla ya Kristo = KK.
Hii ndiyo sababu ya kwamba dunia karibu yote ilikosa kusheherekea mwaka 2000 kuwa mwanzo wa milenia mpya. Mwaka 2000 ulikuwa mwaka wa mwisho wa karne iliyoanza mwaka 1901; karne na milenia mpya zilianza mwaka 2001.
Kosa la Hesabu ya Dionysio
haririHesabu ya Dionysio ilikosea miaka kadhaa. Ni kwa sababu wakati wake Dola la Roma lilikuwa limeshakwisha katika Italia, Kaisari alikaa Bizanti au Roma ya Mashariki. Kumbukumbu za Roma yenyewe hazikutunzwa tangu miaka mingi.
Leo hii wataalamu wengi hukubaliana ya kwamba kasoro Ya Dionysio ni takriban miaka 4 - 8; yaani mwaka halisi wa kuzaliwa kwake Yesu ulikuwa kama miaka nne hadi nane kabla ya mwaka ambao tumezoea kuhesabu kama "1", kwa kuwa mwaka 4 K.K. ndipo alipokufa mfalme Herode Mkuu aliyejaribu kumuua akiwa mtoto mchanga.
Wengi walijaribu kusahihisha kosa hilo lakini habari kamili kabisa haziwezi kupatikana, tena ni vigumu kubadilisha mahesabu yote, vitabu n.k.
Uenezi wa Hesabu "Kabla ya / Baada ya Kristo"
haririMwanzoni hesabu ya Dionysio ilikuwa pendekezo la mtaalamu fulani tu, watu wakiendelea kutumia mahesabu yao mbalimbali.
Miaka 60 baada ya Dionysio, Papa Bonifas IV, akiwa mkuu wa Kanisa Katoliki, alitumia tarehe zote mbili za "baada ya Kristo" na "tangu kuanzishwa kwa mji". Wataalamu walianza kutumia zaidi hesabu hiyo mpya.
Mnamo mwaka 725 mtaalamu Beda Mheshimiwa alitunga kitabu "Kuhusu ugawaji wa wakati" (kwa Kilatini De Temporum Ratione) alikotumia mfumo ulioundwa na Dionysio akaendelea kuutumia pia katika kitabu kuhusu "Historia ya Kanisa". Kwa kuwa vitabu vya Beda vilikuja kutumiwa kote katika Ulaya ya Magharibi, vilichangia sana uenezi wa hesabu hiyo mpya.
Wakati wa Karolo Mkuu, Mfalme (halafu Kaisari) aliyetawala Ufaransa pamoja na Ujerumani, Italia ya Kaskazini na maeneo ya Uholanzi na Ubelgiji, hesabu tangu Kristo ilikuwa rasmi kwa serikali.
Lakini bado zilihitajika karne kadhaa hadi hesabu hii iwe imekuwa kawaida katika Ulaya.
Kutokana na uenezaji wa uchumi, biashara na utawala wa Wazungu, hesabu "Baada ya Kristo" ilienea kote duniani.
Siku hizi ni hesabu pekee katika nchi nyingi. Katika nchi mbalimbali inatumika sambamba na mahesabu mengine.
Nchi mbalimbali za Kiislamu hutumia miaka tangu Hijra ya Muhammad (mwaka 622 BK), lakini mara nyingi pamoja na miaka ya hesabu ya Kikristo kwa ajili ya mambo ya biashara na mawasiliano ya kimataifa.
Nchi ya Israeli inatumia kalenda rasmi tangu "kuumbwa kwa dunia", isipokuwa kando ya Kalenda ya BK kwa sababu zilizotajwa hapo juu kwa ajili ya nchi za Kiislamu.
Japan inatumia hesabu ya miaka ya Kaisari yake - vilevile kando ya Kalenda ya BK.
Namna za kutaja Hesabu "Kabla ya / Baada ya Kristo"
haririDionysio hakutumia msamiati "baada ya Kristo" - alisema "Anno Domini" ("mwaka wa Bwana") akimaanisha Dominus = Bwana ndiye Yesu. Hivyo kifupi katika lugha ya Kilatini ni "AD" kilichoingia pia katika Kiingereza na lugha nyingine kadhaa.
Hata miaka kabla ya Kristo kwa Kiingereza huitwa kwa kifupi cha Kilatini "a. Chr" (ante Christum natum = kabla ya kuzaliwa kwake Kristo). Wengine hutumia "BC" = "before Christ".