Jump to content

Draft:UPOTOSHAJI KWENYE KISWAHILI

From Wikipedia, the free encyclopedia

This is an old revision of this page, as edited by Dee Soulza (talk | contribs) at 19:10, 20 March 2024 (Added more content). The present address (URL) is a permanent link to this revision, which may differ significantly from the current revision.


Kiswahili ni moja ya lugha kumi maarufu zinazozungumzwa na watu wengi duniani. Ni lugha ya Wabantu wa asili ya Afrika Mashariki ambayo kwa sasa mawanda yake yamepitiliza nje ya eneo hilo la kijiografia.

Kwa sasa (ikiwa ni mwaka 2024), lugha ya Kiswahili imeshakuwa ni lugha rasmi ya kikazi kwa Umoja wa Afrika (African Union), Jumuia ya Maendeleo ya Kusini kwa Afrika ("SADC") na Jumuia ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki ("EAC"). Hii inadhihirisha hadhi na umuhimu wa lugha ya Kiswahili.

Pamoja na kukua, kusambaa, kupevuka na kupanda hadhi kwa lugha hii kama ilivyoelezwa hapo juu, Kiswahili kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali na katika makala hii, jambo linalojadiliwa ni juu ya upotoshaji unaokikabili.

Upotoshaji wa Maana za Maneno

Baadhi ya watumiaji wa lugha hii wamekuwa wakipotosha maana za maneno mbalimbali, ama kwa kutofahamu maana asilia za maneno hayo au kwa kutokuwa waangalifu katika matumizi yake. Mfano mzuri, ni pale neno sura linapotumika kumaanisha 'uso' kama katika: nitaiweka wapi sura yangu (badala ya: nitauweka wapi USO wangu). Mfano mwingine ni matumizi ya neno 'binti' kusimama mahala pa 'msichana' (si kweli kuwa kila binti ni msichana au kila msichana ni binti wa mzungumzaji).

Upotoshaji wa Maana za Methali, nahau, nk.

Maana za methali, nahau, tamathali za semi, nk. pamoja na maumbo yao ya asili, hayana budi kuhifadhiwa. Kwa mfano, methali "kufa kufaana" imepotoshewa maana yake na kuwa: afapo mtu, kunapatikana fursa mbalimbali kwa waliobaki hai kama vile kurithiwa mali, cheo, nk. Lakini maana yake sahihi ni: patokeapo msiba, ndugu na majirani husaidiana (hufaana). Upande mmoja ukifikwa na msiba, mwingine utatoa msaada, na kinyume chake.

Kadhalika, baadhi ya methali zinaharibiwa maumbo yao ya asili. Kwa mfano, 'mali bila daftari hupotea bila habari' hubadilishwa na kuwa 'mali bila daftari hupungua bila habari' (Daftari husisitiza uwekaji wa kumbukumbu na kujua kipi kimekwenda wapi si kuzuia kutumika kwa vitu hivyo)

Upotoshaji Unaorasmishwa

Hutokea hivi: afisa kutoka baraza linalolea na kukisimamia Kiswahili, kwa kutong'amua kuwa hayupo sahihi, anauambia umma kupitia vyombo vya habari kuwa si sahihi kusema "bahati mbaya" bali waseme "isivyo bahati" kwani neno bahati lina maana chanya na bahati haiwezi kuwa mbaya.

Utetezi wa hoja hii ni kama ifuatavyo: kirai au kifungu cha maneno, 'bahati mbaya' pamoja na visawe vyake katika lugha mbalimbali duniani, kina maana ya kinahau (idiomatic meaning) na hakichambuliwi (intact phrasing) neno kwa neno ili kuipata maana. Pia inakuwa dhahiri kuwa katika hali hiyo, mtaalamu anakuwa anawaza kwa Kiingereza na kukanganya msamiati 'unfortunate' na kirai 'bahati mbaya' cha Kiswahili. Kiingereza cha bahati mbaya ni 'bad luck'. Tunaweza kukubali japo kwa shingo upande kuwa tafsiri ya 'unfortunate' ni 'isivyo bahati'

Tuangalie visawe vya bahati mbaya katika lugha mbalimbali (zote zina maneno mawili: bahati na mbaya);

Kiingereza _ bad luck

Kifaransa _ mal chance

Kiganda _ emikisa emibi

Kilingangala _ makila mabe/ chance ya mabe

Kispaniola _ mala suerte

Kireno _ mà sorte

Kiarabu _ Haza sayi

Upotoshaji wa Waandishi Huru

Kuna athari juu ya Kiswahili zinazotokana na uandishi huru wa mtandaoni. Hii inajumuisha waandishi wote ambao huanikiza mawazo yao kwa jamii bila kulazimika kuyapitisha kwa wahariri rasmi au wao wenyewe kuwa na taaluma ya uandishi. Mifano ni Waandishi kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, WhatsApp, TikTok, nk.; tuvuti mbalimbali, blogu na majukwaa mengine. Namna zote hizo za uwasilishaji maudhui kupitia wavuti, zina athari kubwa kwa Kiswahili kwani makosa mengi hufanyika kwa kukosekana udhibiti wa ubora wa lugha. Kuna makosa ya upotoshaji wa tahajia, matamshi, utumiaji ndivyo - sivyo wa misamiati na sintofahamu kadha wa kadha za kisarufi na kifasihi.

Hitimisho:

Wito unatolewa kwa wadau wa Kiswahili kujitolea katika kufanya tafiti ndogondogo zitakazobaini changamoto za Kiswahili hususan zinazohusiana na upotoshaji na kupendekeza hatua za utatuzi. Kamwe tusichoke kukilea, kukikuza, kukiendeleza na kukitunza Kiswahili.






References